amreezle

amreezle

Monday, February 27, 2012

MZUNGU MWINGEREZA,ALIYEWAI KUWA MBUNGE WA KINONDONI.

Noel Bryceson: Mzungu aliyekuwa mbunge wa Kinondoni
ALIKUWA Mzungu Mwingereza aliyekuwa mbunge wa Kinondoni katika Jiji la Dar es Salaam.  Ni mbunge aliyependwa zaidi na wakazi wa jimbo hilo ambao waliapa kumpa ubunge hadi mwisho wa maisha yake.
Ni hayati Dereck Bryceson, ambaye jina lake kamili alikuwa ni Dereck Noel MacLeod Bryceson aliyekuwa mwanasiasa na waziri katika serikali ya wakoloni wa Uingereza na akawemo kwenye baraza la kwanza la mawaziri la Mwalimu Julius Nyerere wakati wa kupata uhuru.
Mzungu huyo kipenzi cha Waswahili, alipewa jina la ‘Mbunge wa Maji’ kwani ndiye aliyeongoza mipango ya kupeleka maji eneo ambalo sasa linaitwa Sinza na alikuwa mstari wa mbele katika upimaji wa viwanja katika kitongoji hicho maarufu kwa ujenzi wa nyumba na taasisi mbalimbali.
Kwa wanaokumbuka, mipango ya kupeleka maji ya bomba Sinza ilianza mapema hata kabla ya watu kupimiwa viwanja eneo hilo.
Hadi Bryceson anafariki, Jumamosi ya Oktoba 11, 1978 katika Hospitali ya Hanover, Ujerumani Magharibi (wakati huo) alikuwa akiwania tena nafasi ya ubunge wa Kinondoni ambao ungefanyika katika uchaguzi wa nne 1980. Alifariki akiwa na umri wa miaka 58.
Tofauti na Wazungu wenzake waliokuwa katika serikali ya Nyerere, Bryceson alikuwa mbunge wa kuchaguliwa kutoka Jimbo la Kaskazini lililojumuisha Mikoa ya Kilimanjaro na Arusha wakati huo.
Bunge wakati huo lilijulikana kama Baraza la Kutunga Sheria yaani Legico, kifupi cha Legislative Council.
Bryceson aliingia Tanganyika kwa mara ya kwanza 1952, akitokea Kenya akiwa mkulima na akiwa na umri wa miaka 38. Alipata elimu katika Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza na akajiunga na kikosi cha Jeshi la Anga la Uingereza wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.
Akiwa rubani wa kijeshi, alipata ajali iliyomletea ulemavu wa kutembea, akaambiwa angetumia kiti cha kusukumwa siku zote.  Lakini kutokana na dhamira yake, alitoka kwenye kiti akawa anatembelea “magongo” na hatimaye fimbo moja tu, japokuwa kwa kusota.
Waliomwona wanakumbuka.
Aliingia katika serikali (ya wakoloni wa Kiingereza) mara ya kwanza 1957 akiwa Waziri Msaidizi wa Kazi za Starehe, baadaye, Juni 1959, akawa Waziri wa Madini na Biashara, na 1960, chini ya  serikali ya Mwalimu Nyerere akiwa Waziri wa Afya na Kazi.
Ni Dereck Bryceson aliyekuwa mtoto wa Bi Norma Bryceson, mume wa Jane Goodall, na kaka wa Michael Bryceson na Peter Bryceson.

No comments:

Post a Comment